MCHEZO WA KIRAFIKI WA SERENGETI BOYS WAFUTWA
Timu ya Vijana ya
Kenya imefuta ziara yake ya kwenda Dar es Salaam kwa ajili kucheza
mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya vijana wa Tanzania wenye umri
wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys.
Mchezo huo ulipangwa kufanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tarehe 23 Julai, 2016.
Kwa
mujibu wa barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Kenya (FKF), Robert Muthomi kwenda Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), kufuta kwa ziara hiyo kunatokana na nafasi ambayo Kenya imeipata
kwingine.
Timu ya Taifa ya Vijana ya Kenya imeteuliwa kushiriki
michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la COSAFA inayotarajiwa kuanza
Julai 22, 2016 hadi Julai 31, 2016 mara baada ya Msumbiji kujitoa kwenye
mashindano hayo.
Licha ya kwamba mchezo huo hautakuwapo, ratiba
ya Serengeti Boys ambayo inapambana kuwania nafasi ya kucheza Kombe la
Mataifa Afrika hapo mwakani, imebaki vilevile kwa timu kuingia kambini
Jumapili Julai 17, 2016 kwenye Hosteli za TFF zilizoko Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo inayonolewa na Bakari Shime itapiga kambi
ya wiki moja katika hosteli hizo, kabla ya kwenda Madagascar ambako
itapiga kambi ya takribani wiki mbili ikiwa ni ahadi ya Rais wa TFF,
Jamal Malinzi ambaye alitoa ofa hiyo baada ya kuwatoa Shelisheli kwa
jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake mbili za kimataifa.
Serengeti
Boys inatarajiwa kucheza na Afrika Kusini kati ya Agosti 5, 6 au 7,
2016 huko Afrika Kusini kabla ya mchezo wa marudiano utakaofanyika saa
9.00 alasiri, Agosti 14, 2016 kwenye Uwanja wa Azam Complex, ulioko
Chamazi, Dar es Salaam.
Mshindi wa jumla katika michezo hiyo, itacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville.
Maoni
Chapisha Maoni