BALE AWAJAZA FURAHA WALES
Meneja wa timu ya
taifa ya kandanda ya Wales Chris Coleman amewahimiza mashabiki wakubali
“kutekwa na furaha ya ufanisi” lakini akasema wachezaji wake hawatafanya
hivyo hadi wafuzu kwa Euro 2016.
Baada ya kucharaza Cyprus 1-0 Alhamisi, Wales watafuzu wakiandikisha ushindi dhidi ya Israel Jumapili.
Coleman
anaamini kufikisha kikomo kipindi cha miaka 58 cha Wales kukosa
kushiriki dimba kubwa itakuwa zawadi kubwa kwa mashabiki wa timu hiyo.
"Ujumbe wangu kwao ni kwamba wasisimke na kutekwa na furaha. Wafurahie hili kwani wamesubiri muda mrefu sana.
“Lakini sisi hatuwezi kutekwa na hilo. Siwezi, wachezaji hawawezi, na wakufunzi pia na hatutatekwa na furaha.”
Coleman
ameongeza kuwa bila kujali kama yeye na wachezaji wake wamechoka
kimwili na kiakili, kwa sasa lazima waangazie kujiandaa kwa mechi hiyo
kubwa ya Jumapili.
"Lazima tutimize matarajio. Tumefanya hivyo
kufikia sasa na twatumai kwamba tutafanya hivyo tena,” mkufunzi huyo wa
umri wa miaka 45 ameongeza.
Wales kwa sasa wamo alama tatu mbele
kileleni Kundi B wakiwa wamesalia na mechi tatu, na wamekaribia sana
kucheza fainali za dimba kubwa tangu kushiriki kwao fainali za Kombe la
Dunia 1958.
Baada ya kukaribisha Israel uwanja wa Cardiff
Jumapili, vijana hao wa Coleman watakuwa na mechi mbili dhidi ya
Bosnia-Herzegovina na moja dhidi ya Andorra Oktoba.
Ushindi dhidi
ya Israel utatosha kuwafikisha Euro 2016, lakini Coleman anasisitiza
wachezaji wake hawawezi kuthubutu kufikiria kwamba washafika Ufaransa.
"Hatuwezi
kuutoroka ukweli. Ukiangalia kundi letu lilivyo, tunahitaji kushinda
mechi moja tu kujihakikishia nafasi Ufaransa 2016, hilo twajua,”
akasema.
"Lakini wachezaji, nakuahidi, hawataji hilo kamwe. Wanajua hilo lipo, wanajua kila mtu atakuwa akizungumzia nini nyumbani.
"Waliwaona mashabiki 4,000 waliojitokeza kuwashangilia [Alhamisi], lakini hilo halifai kutufanya tusahau lengo letu.”
Maoni
Chapisha Maoni