TFF WAKANA TUHUMA ZA UFISADI, WAPANGA KUWACHUKULIA HATUA WANAOENEZA

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limepanga kuwafungulia mashataka watu waliosambaza ujumbe ambao sio wa kweli kwenye mitandao ya kijamii kufuatia taarifa walizokuwa wanazisambaza zikidai kuwa shirikisho hilo limeongeza posho za vikao. Akizungumza na wanahabari leo, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao amesema kuwa, amaelazimika kutoa ufafanuzi huo kufuatia hivi karibuni kuwepo kwa taarifa hizo zilizosambaa na kuwa hazina ukweli wowote. Alisema katika taarifa hizo walidai kuwa TFF imeongeza posho kwenye vikao vinavyofanywa na kamati ya utendaji huku kwa mwezi wakipokea kiasi cha milioni moja kila mmoja kwaajili ya mishahara.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred (katikati), akizungumza na wanahabari kwenye Ukumbi wa Hosteli za TFF, Karume mjini Dar es Salaam leo
Mbali na hilo, taraifa hiyo ilieleza kuwa Rais wa TFF, Wallace Karia anapokea kiasi cha milioni 6 wakati makamu wale Richard Wambura, akilamba milioni 5 kwa mwezi kama malipo ya kazi yao. Kidau alisema kuwa, tayari hadi sasa wameshapata majina ya watu 10 ambayo wanaendelea kufuatilia na wengine na baada ya hapo watawafungulia mashtaka. “Kuna taarifa ambazo si za kweli watu wanazisambaza kwenye mitandao ya Kijamii na sasa hivi kuna sheria za mitandao, leo baada ya kikao hiki tunaenda kuwafungulia mashtaka watu waliohusika na jambo hili kwa kueneza vitu ambavyo sio vya kweli,” amesema Kidao. Alisema wataendelea kufuatilia kila mtu aliyehusika kwa maana ya aliyetuma ujumbe huo kwani kwa sasa wanazo baadhi ya namba na watazichapisha.
Rais wa TFF, Wallace Karia (kushoto) anajikuta katika mtihani wa kwanza miezi mitatu tu tangu aingie madarakani
WARAKA WA TUHUMA UNAZOSAMBAZWA NI HUU; “KAMATI TENDAJI YA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF) KUTUMIA MILIONI 438 KWA MWAKA  KUJILIPA POSHO. Tarehe 28/10/2017 Kamati ya Utendaji ya TFF, ilifanya Kikao katika Hoteli ya SEA SCAPE Kunduchi Beach jijiji Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine ilipitisha azimio la Wajumbe wa Kamati hiyo kuanza kulipwa posho  ya kila mwezi kwa mchanganuo ufuatao:  1. Rais wa  TFF  Tsh.Mil.6 kwa mwezi  sawa na Mil.72 kwa Mwaka. 2. Makamu wa Rais wa TFF, Tsh. mil. 5  kwa mwezi sawa na Mil.60 kwa mwaka. 3. Wajumbe 20 wa Kamati ya Utendaji kila mmoja Tsh. Mil. 1 kwa mwezi sawa na mil.12 kwa mwaka ,  kwa wajumbe 20 ni Tsh.  Mil. 240 kwa mwaka. NB: Posho hizi ni mpya na hazijawahi kuwepo katika shirikisho hilo katika uongozi uliopita.   Aidha Posho za kila kikao zimepanda kutoka Tsh. 300, 000/=  uongozi uliopita hadi laki tano (500,000/) uongozi wa sasa kwa kila mjumbe,  kwa mwaka kuna vikao vya kawaida visivyopungua sita,  kwa Wajumbe wote 22 kwa mwaka itakuwa mil.66.  Kwa  mchanganuo huo, Gharama za Posho tu kwa mwaka kwa Wajumbe wa  Kamati ya Utendaji tu ni milioni mia nne thelathini na nane (mil.438). Bado posho za vikao vya dharura, posho za watumishi wengine n.k Moja ya changamoto za maendeleo ya Mpira wa Miguu Tanzania ni Ukosefu wa fedha.  Timu zetu za taifa zinashindwa kukaa kambini,  Waamuzi wanakosa Mafunzo, viwanja vya michezo vinashindwa kuboreshwa, vilabu vya michezo havisaidiwi na mambo mengine chungu nzima hayafanyiki sababu ya ukosefu wa fedha, leo hii EXCOM  inakwenda kujifungia Sea ESCAPE na kuidhinisha  mil. 438 kwa ajili kujilipa posho!  Kwa mwendo huu tusitegemee maendeleo katika soka Tanzania. Rais wa TFF,  WALES KARIA na Makamu wake, MICHAEL WAMBURA wanapaswa kujitathmini upya,”. 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii