BAO LA UTATA LAWAONDOA SERENGETI BOYS GABON
Tanzania imetolewa katika michuano
ya vijana chini ya umri wa miaka 17, baada ya kufungwa 1-0 na Niger
katika mchezo wa mwisho wa Kundi B Uwanja wa Port Gentil mjini Gentil,
Gabon.
Matokeo hayo yanazifanya Niger na Tanzania zifungane pointi
na wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo mshindi katika mechi
baina yao anafuzu Kombe la Dunia Oktoba mwaka huu India na pia kwenda
Nusu Fainali ya michuano hiyo.
Niger anaungana na Mali iliyoongoza
kundi kwa pointi zake saba, baada ya ushindi wa mechi mbili na sare
moja, wakati Tanzania na Angola zote zinatolewa.
Katika mchezo huo
uliochezeshwa na refa Daniel Laryea wa Ghana, aliyesaidiwa na Seydou
Tiama wa Burkina Faso na Attia Amsaad wa Libya, Niger walipata bao lao
kipindi cha kwanza, mfungaji Ibrahim Boubacar Marou dakika ya 41 baada
ya shambulizi zuri lililowachanganya walinzi wa Serengeti Boys.
Lakini
Niger wangetoka uwanjani wanaongoza kwa mabao zaidi baada ya dakika 45
za kipindi cha kwanza kama si umahiri wa kipa Ramadhan Awam Kabwili
kuokoa michomo zaidi ya mitatu ya wazi.
Kwa ujumla, Serengeti Boys
ilizidiwa mchezo kipindi cha kwanza na kipindi cha pili hali iliendelea
kuwa hivyo na hatimaye Niger wakaitoa Tanzania. Wachezaji wa Tanzania
walikuwa wenye huzuni baada ya mchezo huku wakilia.
Mbali na Mali na Niger, timu nyingine zilizofuzu Nusu Fainali ni Ghana na Guinea kutoka Kundi A.
Kikosi
cha Tanzania kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Ally Ng'anzi, Nickson
Kibabage, Dickson Job, Abdul Suleiman, Asad Ali/Muhsin Makame dk85,
Kibwana Ally, Shaaban Zuberi, Ally Msengi, Ibrahim Abdallah/Yohanna
Nkomola dk46 na Kelvin Naftal.
Niger; Khaled Ibrahim, Yacine
Massamba, Habibou Sofiane, Rachid Souley, Abdoul Karim, Djibrilla
Ibrahim, Inoussa Amadou, Abdoul Rachid, Ibrahim Boubacar, Ibrahim Namata
na Hamid Galissoune Ajina.
Maoni
Chapisha Maoni