TAIFA STARS YAAMBULIA KICHAPO ALGERIA


Michezo ya raundi ya pili ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Urusi 2018 kwa ukanda wa Afrika, ilichezwa jana huku timu za Tanzania, Kenya na Rwanda zikishindwa mechi zao.
Tanzania wakicheza ugenini dhidi ya Algeria walikubali kichapo cha mabao 7-0 na kufuta kabisa ndoto yao ya kusonga mbele.
Mambo yalianza kuwaendea mrama Taifa Stars dakika ya kwanza Mudathir Yahya Abbas alipoonyeshwa kadi ya njano ambayo baadaye iliwauma pale alipoonyeshwa kadi nyingine ya njano dakika ya 41 na kufukuzwa uwanjani.

Stars walilazimika kucheza kipindi cha pili wakiwa wachezaji kumi.

Dakiak hiyo hiyo ya kwanza, nyota wa Algeria anayechezewa FC Porto ya Ureno Yacine Brahimi aliwafungia mbweha wa jangwani bao la kwanza.

Algeria walifunga bao la pili dakika ya 23 kupitia Ghoulam ambaye pia aliwafungia dakika ya 59 kupitia mkwaju wa penalti.

Mabao hayo mengine ya Algeria yalifungwa na Riyad Mahrez (43), Islam Slimani (49, 75) na Carl fMedjani (72).

Tanzania walibanduliwa kutoka kwa kinyang'anyiro hicho cha kuelekea Urusi kwa kushindwa kwa jumla ya mabao 9-2 baada yao kutoka sare ya 2-2 mechi ya mkondo wa kwanza jijini Dar es Salaam.

Timu ya taifa ya Kenya Harambee Star nao wakalala kwa kufungwa mabao 2-0 na Cape Verde.

Mabao ya Cape Verde yalifungwa na Heldon Ramos dakika ya 45 na dakika ya 52 na wakabanduliwa kwa jumla ya 2-1 baada yao kushinda 1-0 mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezewa Nairobi.

Rwanda nao wakicheza katika uwanja wao wa nyumbani Kigali walifungwa na Libya kwa mabao 3-1. Mounir alifungia Libya bao la kwanza dakika ya 36, la pili wakafungiwa na Mohamed Ghanudi dakika ya 48 na kisha Mounir akaongeza la tatu dakika ya mwisho.

Bao la kufutia machozi la Rwanda lilifungwa na Jacques Tusiyenge dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza.

Rwanda walibanduliwa kwa kushindwa kwa jumla ya 1-4 baada yao kulazwa 0-1 mechi ya mkondo wa kwanza ugenini.

Matokeo mengine ya mechi zilizochezwa Jumanne ni kama ifuatavyo:

Cameroon 0-0 Niger (Jumla 3-0)

Congo 2-1 Ethiopia (Jumla 6-4)

Nigeria 2-0 Swaziland (Jumla 2-0)

Ghana 2-0 Comoro (Jumla 2-0)

Misri 4-0 Chad (Jumla 4-1)

Ivory Coast 3-0 Liberia (Jumla 4-0)

Tunisia 2-1 Mauritania (Jumla 4-2)

Afrika Kusini 1-0 Angola (Jumla 4-1)

Burkina Faso 2-0 Benin (Jumla 3-2)

Senegal 3-0 Madagascar (Jumla 5-2)

Mali 2-0 Botswana (Jumla 3-2)

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii