ISSA HAYATOU RAIS WA FIFA
Kiongozi wa
shirikisho la soka barani Afrika Issa Hayatou kutoka Cameroon amepewa
jukumu la kuongoza shirikisho la soka duniani Fifa kwa muda.
Hayatou
atachukua usukani kufuatia kusimamishwa kazi kwa Rais wa Fifa Sepp
Blatter kwa muda wa siku 90 na Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo,
shirikisho hilo linalosimamia soka duniani limesema kupitia taarifa.
Hayatou,
aliyeongoza CAF tangu 1988, atachukua usukani kwa mujibu wa sheria za
Fifa, akiwa ndiye makamu wa rais katika kamati tendaji ya Fifa
aliyehudumu muda mrefu zaidi.
Baadaye, Hayatou ametoa taarifa na kusema amepokea majukumu hayo mapya lakini ataongoza tu kwa muda.
“Rais mpya atachaguliwa kwenye Mkutano Mkuu Februari 26, 2016. Na mimi mwenyewe sitawania,” amesema kupitia taarifa.
“Hadi
mkutano huo ufanyike, naahidi kwamba nitajitolea kwa nguvu zangu zote
kutumikia shirikisho hili, mashirikisho wanachama, waajiri wetu,
washirika na mashabiki wa soka popote walipo.”
Aidha, ameahidi
kuendelea kushirikiana na watawala na kuendeleza uchunguzi kwenye
shirikisho hilo lililoyumbishwa na madai ya ulaji rushwa.
Maoni
Chapisha Maoni