SIMBA VS YANGA HAPATOSHI TAIFA LEO


WATANI wa jadi, Simba na Yanga SC wote walirejea jana Dar es Salaam kutoka kwenye kambi zao Zanzibar kuelekea pambano lao la leo.
Miamba hiyo inatarajiwa kumenyana leo jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanzia Saa 10:00.
Yanga SC ilikuwa imeweka kambi kisiwani Pemba wakati mahasimu wao, Simba SC walikuwa Unguja kwa wiki yote hii kujiandaa na mchezo huo.
Hakuna majeruhi wa kutisha katika kambi zote mbili na makocha wote, Muingereza Dylan Kerr wa Simba SC na Hans van der Pluijm wa Yanga SC wamefurahia maandalizi yao.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezeshwa na refa mwenye beji ya Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA), Israel Mujuni Nkongo wa Dar es salaam, atakayesaidiwa na Josephat Bulali wa Tanga, Ferdinand Chacha wa Mwanza, wakati mezani atakuwapo Soud Lila pia wa Dar es Salaam na Kamisaa atakuwa Charles Mchau kutoka Kilimanjaro.
Viingilio katika mchezo huo vinatarajiwa kuwa Sh 7,000 kwa kwa viti vya rangi ya bluu, kijani na chungwa, Sh. 30,000 kwa VIP A na Sh. 20,000 kwa VIP B na C, wakati tiketi zimeanza kuuzwa tangu asubuhi ya jana katika vituo vya Ofisi za TFF Uwanja wa Karume, Buguruni – Oilcom, Dar Live – Mbagala, Uwanja wa Taifa, Luther House – Posta, Feri – Kivukoni, Mnazi Mmoja, Ubungo – Oilcom na Makumbusho – Standi ya mabasi ya daladala.
Watani hao wa jadi, wanakutana leo baada ya wote kuwa na mwanzo mzuri katika Ligi Kuu, wakishinda mechi zao zote tatu za awali, Yanga ikizifunga 2-0 Coastal Union, 3-1 Prisons na 4-1 JKT Ruvu, wakati Simba ilizifunga 1-0 African Sports, 2-0 Mgambo JKT na 3-1 Kagera Sugar.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii