MKWASA KUPATA ULAJI WA KUDUMU STARS
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) lipo katika mchakato wa kumpa Mkataba wa kudumu, kocha wa muda wa timu ya taifa, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa.
Pamoja na kucheza mechi tatu bila kushinda, lakini TFF imeridhishwa na maendeleo ya timu kutoka ilivyokuwa chini ya kocha Mholanzi, Mart Nooij na imeshawishika kumpa Mkataba wa kudumu Mkwasa.
Kiwango kizuri ambacho timu ilionyesha katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Nigeria kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ndicho kimeifanya TFF ifikirie hilo.
Aidha, TFF pia baada ya kukusanya maoni ya wachezaji mmoja na wote kuridhishwa na benchi la Ufundi la sasa la timu- inaona hakuna sababu ya kutowapa Mkataba wa kudumu Mkwasa na benchi lake.
Washambuliaji wawili wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta pamoja na Nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga SC ya nyumbani walisema timu imebadilika chini ya Mkwasa.
Viungo Himid Mao wa Azam FC na Said Ndemla wa Simba SC nao walisema timu imebadilika mno kutoka ilivyokuwa chini ya Nooij.
Lakini inafahamika Mkwasa ni kocha wa Yanga SC anayefanya kazi na Mholanzi, Hans van der Pluijm na kuhusu hilo, klabu hiyo imesema haina shida kumuachia.
Katibu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha amesema kwamba wako tayari kumuachia Mkwasa akafanye majukumu ya kitaifa.
“Tunachoomba tu TFF wafuate utaratibu wa kuvunja mkataba, ana Mkataba na sisi wa miaka miwili, ambao ameutumikia kwa miezi minane tu,”amesema Tiboroha.
Maoni
Chapisha Maoni